Polisi nchini India waliwakamata watu kadhaa mjini New Delhi siku ya Jumamosi, na kuvuruga siku ya pili ya maandamano dhidi ya mabadiliko ya daftari la wapiga kura. Maandamano hayo yanaungwa mkono na chama cha Cockroach Janta Party, kinachoongozwa na vijana wa kizazi cha Gen Z, pamoja na makundi mengine ya upinzani.
Waandamanaji wanadai kuwa mabadiliko hayo yanakinufaisha chama tawala cha Waziri Mkuu Narendra Modi, na wanataka mkuu wa tume ya uchaguzi ya India ajiuzulu.
Maandamano haya ni ya karibuni zaidi katika mfululizo wa maandamano yanayoongozwa na vijana yaliyoibuka mwaka huu, na yanamweka Modi chini ya shinikizo ambalo hajawahi kukabiliana nalo katika miaka yake 12 madarakani.
Siku ya Jumamosi, takriban waandamanaji 100 waliondoa vizuizi vya usalama na kuimba “mwizi wa kura, ondoka madarakani” na “Gyanesh Kumar, jiuzulu,” kabla polisi hawajawakamata baadhi yao kwa nguvu.
Kwa mujibu wa shahidi wa Reuters, miongoni mwa waandamanaji walikuwemo Mbunge huru Kapil Sibal, Rais wa chama cha wanafunzi cha mrengo wa kushoto All India Students' Association, Neha Bora, pamoja na wanaharakati wa kisiasa Prashant Bhushan na Yogendra Yadav. Polisi walikataa kutoa maoni kuhusu idadi na utambulisho wa waliokamatwa.
“Kwanza waliwaondoa watu kwenye daftari la wapiga kura, na sasa hawaturuhusu kupaza sauti zetu dhidi ya hili. Hili halikubaliki,” Bora aliiambia Reuters.
Mkuu wa Tume ya Uchaguzi, Kumar, hajatoa kauli yoyote kuhusu maandamano hayo wala madai ya kumtaka ajiuzulu.
Siku ya Ijumaa, polisi waliwazuia kundi la waandamanaji kukusanyika na kuwasukuma ndani ya mabasi. Vituo kadhaa vya treni za mjini (metro) vilivyo karibu vilibaki vimefungwa huku ulinzi ukiwa umeimarishwa.
Kwa mujibu wa chanzo kimoja cha polisi, ingawa wengi wa waliokamatwa Ijumaa waliachiliwa, baadhi yao walifunguliwa mashtaka ya madai ya kukiuka amri zinazopiga marufuku mikusanyiko mikubwa mjini Delhi.
Wakosoaji wanasema zoezi la kitaifa la kuhakiki wapiga kura lililoanzishwa mwaka jana limesababisha mamilioni ya wapiga kura halali kuondolewa kwenye daftari la wapiga kura.
Kwa upande wake, tume hiyo, ambayo kwa muda mrefu imechukuliwa kuwa mojawapo ya taasisi zinazoaminika zaidi nchini, inasema zoezi hilo linalenga kuondoa majina yaliyojirudia, ya watu waliofariki na ya wasiostahili kupiga kura. Siku ya Ijumaa, tume iliwaagiza maafisa kuwasajili wapiga kura wapya waliofikia sifa pamoja na wale walioachwa nje ya daftari.
Comments
0