Aliyekuwa Rais wa Brazil, Jair Bolsonaro, amelazwa katika chumba cha wagonjwa mahututi (ICU) katika hospitali ya DF Star iliyoko mji mkuu, Brasilia. Hospitali hiyo ilithibitisha taarifa hizo kupitia taarifa rasmi iliyotolewa Jumamosi.
Siku ya Ijumaa, madaktari waligundua kuwa Bolsonaro alikuwa na tatizo la kuziba kwa ghafla tumboni mwake.
Wataalamu wa afya wameanza matibabu ya kuhakikisha mwili wake unapata maji ya kutosha, na amewekewa mrija wa tumbo (gastric tube).
Kwa mujibu wa hospitali, hali ya rais huyo wa zamani ni tulivu kitabibu na yuko na fahamu, lakini kwa sasa hakuna tarehe inayotarajiwa ya kuruhusiwa kutoka hospitalini.
Bolsonaro, aliyeongoza Brazil kuanzia mwaka 2019 hadi 2022, amekuwa akilazwa hospitalini mara kwa mara na kufanyiwa upasuaji kadhaa kutokana na jeraha la kuchomwa kisu tumboni wakati wa tukio la kampeni mwaka 2018.
Tangu mwaka jana, Bolsonaro amekuwa akitumikia kifungo cha miaka 27 jela kwa kupanga mapinduzi baada ya kushindwa katika uchaguzi wa mwaka 2022 na Rais wa sasa, Luiz Inacio Lula da Silva.
Comments
0