Somalia imemwamuru balozi wa Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE) kuondoka nchini humo ndani ya saa 72, na pia imemrejesha nyumbani balozi wake kutoka Abu Dhabi. Katika uamuzi uliotangazwa Alhamisi, serikali ya Mogadishu iliishutumu UAE kwa ukiukaji wa mamlaka yake ya kujitawala ambao haukufafanuliwa, ikisema vitendo hivyo ni sawa na “uvamizi wa wazi.”
Waziri wa Habari Abdifatah Kasim Mohamud, akizungumza kupitia shirika la habari la serikali, alionya: “Hatua zitachukuliwa dhidi ya yeyote atakayeshirikiana na UAE katika uvamizi dhidi ya Somalia.”
Aliongeza: “Wasomali wote wanahimizwa kuilinda nchi yao na kuungana dhidi ya uvamizi wa wazi wa UAE dhidi ya mamlaka, usalama, ardhi na umoja wa Wasomali.”
Waziri huyo hakueleza ni hatua zipi hasa za UAE zilizosababisha uamuzi huo. Hata hivyo, katika hotuba yake ya Jumanne, Rais wa Somalia Hassan Sheikh Mohamud aliishutumu UAE kwa kuzipa baadhi ya serikali za majimbo ya Somalia msaada wa kiuchumi na kisiasa ili kuipinga serikali ya shirikisho.
UAE, ambayo hapo awali imesaidia kufadhili na kutoa mafunzo kwa jeshi la Somalia, na imeunga mkono bandari pamoja na miradi mingine ya kibiashara nchini humo, kwa muda mrefu imekanusha madai ya kuingilia masuala ya ndani ya nchi hiyo.
Siku ya Alhamisi, msemaji wa wizara ya mambo ya nje ya UAE alilaani kile alichokiita mtazamo wa serikali ya Somalia “wa kuchochea mvutano na wa uhasama” dhidi ya UAE. Katika taarifa yake, wizara hiyo ilisikitishwa na kile ilichokieleza kuwa ni juhudi za serikali ya Somalia za kuiingiza UAE katika mapambano yake ya ndani ya kuwania madaraka, ikionya kuwa hatua hizo zinaweza kudhuru maslahi ya nchi zote mbili.
Wizara hiyo ilieleza kuwa UAE ilifunga ubalozi wake mjini Mogadishu na kuwaondoa wanadiplomasia wake mnamo Januari 2026 kutokana na kile ilichokiita vitendo vya uhasama vya serikali ya Somalia, ikiwemo kufutwa kwa mikataba ya pande mbili. Hata hivyo, ilisisitiza kuwa UAE imejitolea kudumisha na kuimarisha uhusiano wake na watu wa Somalia.
Mnamo Januari, Somalia ilitangaza kusitisha mikataba yote na UAE, ikiwemo mikataba ya bandari na ushirikiano wa ulinzi na usalama, ikiishutumu UAE kwa kudhoofisha mamlaka yake ya kitaifa. Wakati huo, majimbo matatu ya Somalia yanayojitawala na yenye uhusiano wa karibu na UAE yalipuuza uamuzi huo.
Kwa muda mrefu, UAE imetumia utajiri wake kupanua ushawishi wake katika eneo la Pembe ya Afrika, ikichanganya nguvu za kiuchumi, kijeshi na kidiplomasia ili kujiimarisha kama taifa lenye nguvu katika ukanda huo.
Kati ya mwaka 2014 na 2018, UAE ilitoa mafunzo kwa mamia ya wanajeshi wa Somalia, na hadi sasa inaendelea kulipa mishahara na kutoa huduma za usafirishaji (logistics) kwa takriban polisi wa kijeshi na wanajeshi wa vikosi maalum 3,400 wa Somalia walioko ndani na pembezoni mwa mji mkuu, kwa mujibu wa vyanzo vya ngazi za juu nchini Somalia.
UAE pia imejenga uhusiano wa moja kwa moja na serikali za majimbo, ikiahidi mamia ya mamilioni ya dola za Marekani kwa ajili ya bandari na miundombinu ya kijeshi katika pwani iliyo kando ya njia za kimataifa za meli.
Kwa miongo kadhaa, serikali ya shirikisho ya Somalia imekuwa na mamlaka finyu kote nchini, na imeshindwa kuwashinda wanamgambo wa Kiislamu licha ya miaka mingi ya msaada wa kimataifa, ukiwemo wanajeshi wa kulinda amani wa Afrika na mashambulizi ya anga ya Marekani.
Comments
0