Wanasiasa kadhaa wenye malengo makubwa ndani ya chama cha Republican wanajipanga kumpa changamoto Makamu wa Rais wa Marekani, JD Vance, katika uchaguzi wa urais wa mwaka 2028, kufuatia hasara kubwa iliyokikumba chama hicho katika chaguzi za Jumanne.
Gavana wa Florida, Ron DeSantis, ameanzisha kampeni kubwa ya kujitokeza kwenye vyombo vya habari katika siku za hivi karibuni huku akijiandaa kwa uwezekano wa kuwania urais, kwa mujibu wa watu watatu waliopewa taarifa kuhusu mipango yake.
Gavana wa Georgia, Brian Kemp, naye anatafakari kuwania urais, kwa mujibu wa mtu mmoja anayefahamu mipango yake.
Wakati huohuo, Seneta wa Texas, Ted Cruz, anapanga kushirikiana na mshauri wa siasa wa muda mrefu, Jeff Roe wa kampuni ya Axiom Strategies, iwapo ataamua kuingia kwenye kinyang’anyiro hicho, kwa mujibu wa watu wawili wanaofahamu fikra zake.
Watu hao, pamoja na wengine waliohojiwa, walizungumza kwa sharti la kutotajwa majina kwa kuwa walikuwa wakizungumzia mazungumzo ya faragha.
Hamasa inayoongezeka ya kumpinga Vance inakuja wakati ambapo maswali yanaibuka kuhusu mwelekeo wa baadaye wa chama cha Republican chini ya Rais Donald Trump, kufuatia matokeo mabaya ya chama hicho katika uchaguzi.
Wakati Vance bado hajaamua iwapo atawania urais mwaka 2028, wapinzani watarajiwa wanaamini kuwa hasara za Republican zimefungua fursa ya kumpa changamoto makamu huyo wa rais aliye madarakani.
Vance pia anakabiliwa na kibarua cha kujitofautisha na Trump, ambaye kushuka kwa umaarufu wake kunaweza kutatiza matumaini ya Vance ya kupata tiketi ya chama cha Republican kuwania urais.
Kinyang’anyiro hiki kinatarajiwa kuamua si tu nani atakuwa mpeperushaji bendera ajaye wa chama cha Republican katika urais, bali pia mwelekeo wa kisiasa wa chama hicho katika zama za baada ya Trump.
Comments
0