Raia wa Bulgaria walijitokeza vituoni siku ya Jumapili kumchagua rais, baada ya duru ya kwanza iliyofanyika wikendi iliyopita kushindwa kutoa mshindi wa moja kwa moja kati ya wagombea wawili wakuu wanaowania nafasi hiyo, ambayo kwa kiasi kikubwa ni ya kiheshima.
Rais aliye madarakani, Iliana Iotova, mwenye umri wa miaka 61, aliongoza mbele ya aliyekuwa waziri mkuu wa mpito, Andrey Gyurov, mwenye miaka 50. Hata hivyo, hakufikia kiwango cha asilimia 50 kinachohitajika katika duru hiyo ya kwanza iliyoshirikisha wagombea 27, na ambayo ilishuhudia idadi ndogo zaidi ya wapiga kura kuwahi kurekodiwa.
Kura za maoni za wapiga kura wanapotoka vituoni (exit polls) zitatangazwa baada ya upigaji kura kufungwa saa mbili usiku (1800 GMT), huku matokeo rasmi yakitarajiwa siku ya Jumatatu kadiri kura zinavyohesabiwa.
Uchaguzi huu unafanyika wakati ambapo, katika mwezi uliopita, meli kadhaa za kibiashara zimeshambuliwa kwa droni katika pwani ya Bulgaria ya Bahari Nyeusi. Mashambulizi hayo yamelaaniwa kimataifa na kuzua wasiwasi kuhusu jinsi vita vya Ukraine vinavyozidi kusambaa.
Inahofiwa kuwa takriban mabaharia ishirini na wanne wamepoteza maisha, na serikali imelazimika kuomba msaada kutoka kwa washirika wake ili kuimarisha usalama wa baharini. Siku ya Jumatano, meli ya makontena ya Ugiriki ilizama baada ya kushambuliwa na droni za baharini.
Wagombea wote wawili wakuu wamelaani mashambulizi hayo na kutoa wito wa kumalizwa kwa vita kwa njia ya kidiplomasia. Waziri Mkuu Rumen Radev, anayemuunga mkono Iotova, alisema matokeo ya mashambulizi hayo “yanalinufaisha Shirikisho la Urusi”.
Iwapo Iotova atashinda, atakuwa mwanamke wa kwanza kuchaguliwa kuwa rais wa Bulgaria. Alikaimu urais mwezi Januari baada ya Radev kujiuzulu ili kugombea na hatimaye kushinda uchaguzi wa bunge, kupitia tiketi ambayo wachambuzi wengi wa siasa waliiona kuwa rafiki kwa Ikulu ya Urusi (Kremlin).
Gyurov, aliyehudumu kama waziri mkuu wa mpito mwaka huu, anaungwa mkono na vyama vinavyoegemea nchi za Magharibi na vinavyopigania mageuzi, na kwa muda mrefu amekuwa akiiunga mkono Ukraine. Akiwa waziri mkuu, alitia saini makubaliano ya ushirikiano wa kiusalama na Kyiv. Wanasiasa kadhaa wa mrengo wa kulia, akiwemo waziri mkuu wa zamani Boiko Borisov, nao wametangaza kumuunga mkono.
Comments
0