Bilionea na aliyewahi kuwa Meya wa Jiji la New York, Michael Bloomberg, amefunga ndoa na mpenzi wake wa muda mrefu, Diana Taylor, wakihitimisha safari ya uhusiano wa miaka 26 kabla ya kuoana.
Bloomberg, mwenye umri wa miaka 84, na Taylor, mwenye umri wa miaka 71, walifunga pingu za maisha Jumatatu katika sherehe ya faragha iliyofanyika nyumbani kwao eneo la Upper East Side jijini Manhattan. Wanafamilia, wakiwemo binti zake Bloomberg, Emma na Georgina, walihudhuria.
Baada ya sherehe hiyo, takriban ndugu na marafiki wa karibu kumi na wawili waliungana na maharusi kwa chakula cha mchana. Hakuna sababu iliyotolewa kuhusu kwa nini harusi ilifanyika wakati huu.
Msemaji wa wanandoa hao alithibitisha ndoa hiyo, akieleza kuwa walikutana kwa mara ya kwanza miaka 26 iliyopita baada ya kupangwa kuketi pamoja kwa bahati.
“Miaka ishirini na sita baada ya mpangilio wa viti wa bahati, Mike Bloomberg na Diana Taylor wamefunga ndoa,” msemaji huyo alisema.
Bloomberg aliongoza Jiji la New York kama meya kwa vipindi vitatu, kuanzia mwaka 2002 hadi 2013. Awali alikuwa amemuoa Susan Brown, na ndoa yao ilidumu kuanzia mwaka 1976 hadi 1993.
Mwaka 2020 aliwania bila mafanikio kuteuliwa kugombea urais kupitia chama cha Democratic, na hadi leo anaendelea kuwa mfadhili mkubwa wa harakati za kisiasa za chama hicho. Timu yake ilisema alichangia takriban dola milioni 80 za Marekani kwa makundi na wagombea wa Democratic katika miezi ya Septemba na Oktoba, kuelekea uchaguzi wa katikati ya muhula nchini Marekani.
Taylor amejijengea taaluma yake mwenyewe katika utumishi wa umma na sekta ya fedha. Aliwahi kuhudumu kama Msimamizi Mkuu wa Benki wa Jimbo la New York chini ya aliyekuwa Gavana George Pataki.
Wakati Bloomberg akiwa meya, Taylor mara nyingi aliandamana naye kwenye hafla rasmi huku akiendelea na shughuli zake za kikazi. Mwaka 2021, aliteuliwa kuwa mwenyekiti wa bodi ya wakurugenzi ya New York City Ballet.
Mara kwa mara, wanandoa hao wamesimulia hadharani visa vya maisha yao. Taylor aliwahi kukumbuka jinsi alivyompa Bloomberg zawadi ya Krismasi mwaka 2007, picha ya watoto wawili wa mbwa aina ya Labrador wenye rangi ya manjano, jambo lililopelekea mbwa hao kuja kuishi nao nyumbani.
Alisema Bloomberg awali aliuliza kama alikuwa na hiari ya kuwakubali mbwa hao, naye akamjibu kuwa alikuwa na hiari, lakini kila uamuzi una matokeo yake.
Taylor pia alimtetea Bloomberg hadharani wakati wa kampeni yake ya urais mwaka 2020, alipokosolewa kwa kauli alizowahi kutoa huko nyuma kuhusu wanawake. Akiwa katika ofisi ya kampeni huko California, alionyesha uungaji mkono wake kwa ujumbe ulioandikwa kwa mkono: “Namkubali Mike, kwa sababu NINAMPENDA MIKE.”
Comments
0