TikTok imetoa ripoti yake ya robo ya pili ya mwaka kuhusu utekelezaji wa Miongozo ya Jumuiya (Community Guidelines Enforcement Report), ikionyesha juhudi zake za kudumu za kujenga mazingira salama na ya kuaminika kwa watumiaji wake.
Kati ya Aprili na Juni 2026, jukwaa hilo liliondoa video 750,185 nchini Kenya kwa kukiuka Miongozo yake ya Jumuiya. Takriban asilimia 99.8 ya video hizo ziliondolewa kabla ya mtu yeyote kuziripoti, na asilimia 93.8 zilishushwa ndani ya saa 24 tangu kuwekwa mtandaoni.
Kwa mujibu wa TikTok, takwimu hizi zinaonyesha uwekezaji wake endelevu katika mifumo ya kisasa ya kugundua maudhui na mbinu za kuchukua hatua haraka, ili kudhibiti kusambaa kwa maudhui yenye madhara.
Katika kipindi hicho, TikTok pia iliondoa zaidi ya akaunti 46,000 nchini Kenya zinazoshukiwa kumilikiwa na watoto walio chini ya umri wa miaka 13, na zaidi ya akaunti milioni 26 duniani kote, kama sehemu ya juhudi za kuwalinda vijana mtandaoni.
Duniani kote, kati ya video zaidi ya bilioni 42.2 zilizochapishwa kwenye jukwaa hilo katika robo ya pili ya 2026, takriban milioni 188.3 ziliondolewa, sawa na karibu asilimia 0.4 ya video zote. Asilimia 99.5 ziliondolewa kabla ya watumiaji kuziripoti, na asilimia 92.7 ndani ya saa 24 baada ya kuchapishwa.
Mifumo ya kiotomatiki iligundua na kuondoa video 183,344,707, na hivyo utekelezaji wa kiotomatiki (mifumo ya kufuatilia mienendo na udhibiti kwa akili bandia, au AI) ulichangia asilimia 97.4 ya uondoaji wote, kiwango cha juu zaidi kuwahi kufikiwa. Aidha, video takriban milioni 6.3 zilirejeshwa baada ya watumiaji kushinda rufaa zao.
TikTok inaendelea kuchukua hatua dhidi ya ukiukaji wa kanuni wakati wa matangazo ya moja kwa moja (LIVE). Nchini Kenya, vyumba 80,640 vya LIVE vilisitishwa kwa kukiuka miongozo ya jukwaa hilo.
Kimataifa, hatua kama maonyo na kunyimwa mapato zilichukuliwa dhidi ya vipindi 47,176,654 vya LIVE na watayarishaji maudhui 26,781,135 kwa kukiuka miongozo ya kupata mapato kupitia LIVE. Maonyo hayo hutumika kuwaelimisha watayarishaji pale maudhui yao yanapoweza kukiuka sera hizo, ili wafanye marekebisho yanayohitajika.
Kadiri zana za AI zinavyozidi kutumika, TikTok inaimarisha juhudi zake za kutambua na kuondoa maudhui yenye madhara au ya kupotosha yaliyotengenezwa kwa AI (AIGC), huku ikiwataka watayarishaji kuweka lebo kwenye maudhui halisi yaliyotengenezwa kwa AI. Nchini Kenya, karibu video 11,000 ziliondolewa chini ya sera yake kuhusu maudhui yaliyohaririwa na AIGC katika kipindi hicho.
Juhudi hizi zinasaidiwa na zana za kuweka lebo kwa watayarishaji, mifumo ya kugundua kiotomatiki, na teknolojia ya C2PA Content Credentials inayowasaidia watumiaji kutambua maudhui yaliyotengenezwa au kubadilishwa kwa kiasi kikubwa kwa kutumia AI.
Ili kuwaelimisha zaidi watumiaji kuhusu matumizi salama ya AI, hivi karibuni TikTok ilizindua nchini Kenya AI Literacy Hub ndani ya programu yake. Kituo hicho kinatoa mwongozo wa jinsi ya kutambua maudhui yaliyotengenezwa kwa AI, kutumia zana za AI kwa uwajibikaji, na kuelewa namna TikTok inavyowezesha matumizi salama ya AI. Kituo hicho kinapatikana duniani kote kwa kutafuta maneno yanayohusiana na AI kwenye jukwaa hilo.
Comments
0