Zambia iko katika mazungumzo na serikali ya Marekani kuhusu mkataba wa madini ya kimkakati (critical minerals), baada ya kuutenganisha na mkataba tofauti wa ufadhili wa sekta ya afya uliosainiwa siku ya Alhamisi, kwa mujibu wa waziri wa mambo ya nje wa nchi hiyo.
Akizungumza katika hafla ya kusaini mkataba wa afya, Waziri wa Mambo ya Nje, Mulambo Haimbe, alieleza kuwa awali kulikuwa na makubaliano mawili yaliyokuwa yakishughulikiwa kwa pamoja.
“Kulikuwa na Mkataba huu wa Makubaliano (Memorandum of Understanding) kuhusu afya na mwingine kuhusu madini ya kimkakati, na tulikuwa tukisema kwamba haya yanahitaji kutenganishwa, na hili limefanyika,” alisema Haimbe.
Chini ya mkataba huo wa afya, Marekani itatoa ufadhili wa dola bilioni 1.5 kwa Zambia.
Zambia ilikuwa imepinga mpango ambao ungeunganisha moja kwa moja ufadhili wa sekta yake ya afya na kuipa Marekani fursa kubwa zaidi ya kufikia madini yake.
Alipoulizwa maelezo zaidi kuhusu mkataba wa madini, waziri huyo alisema bado “unajadiliwa,” lakini hakutoa ufafanuzi zaidi. Pia hakubainisha ni madini gani Zambia inafikiria kuiruhusu Marekani kuyafikia.
Zambia, nchi iliyoko kusini mwa Afrika, ni mzalishaji wa pili kwa ukubwa wa shaba katika Afrika Kusini mwa Jangwa la Sahara, ikitanguliwa na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.
Comments
0