Umoja wa Afrika (AU) unazindua Jumatano shirika la kwanza la bara hilo la kutathmini uwezo wa mikopo (credit rating agency), likilenga kuwa mbadala wa mashirika matatu makubwa ya kimataifa ya tathmini, wakati ambapo mizigo ya madeni inazielemea nchi nyingi za Afrika.
Uzinduzi wa Shirika la Afrika la Kutathmini Uwezo wa Mikopo (AfCRA) utafanyika Port Louis, mji mkuu wa Mauritius, ambako shirika hilo litakuwa na makao yake makuu. Mradi huo umechukua takriban muongo mmoja kukamilika, tangu viongozi wa Afrika walipoidhinisha kuanzishwa kwake mwaka 2018.
“AfCRA inakamilisha mashirika ya kimataifa yaliyopo ya kutathmini uwezo wa mikopo kwa kutoa mtazamo unaotokana na takwimu, utaalamu na hali halisi za Afrika,” Umoja wa Afrika ulisema katika taarifa yake.
Kwa muda mrefu, viongozi wa Afrika wamekuwa wakiyashutumu mashirika ya tathmini ya nchi za Magharibi kwa kushindwa kupima kwa haki hatari ya kuzikopesha nchi za Afrika, na kwa kuharakisha kushusha viwango vyao wakati wa migogoro kama vile vita na milipuko ya magonjwa.
Mashirika hayo yanakanusha ukosoaji huo, yakisema yanatumia mbinu zilezile duniani kote. Uchunguzi wa Reuters wa mwaka 2024 kuhusu mgogoro wa madeni barani Afrika haukupata ushahidi wa upendeleo wa kimfumo katika viwango vilivyotolewa kwa serikali za kanda hiyo na mashirika hayo matatu makubwa ya kimataifa.
Kwa mujibu wa AU, AfCRA itatathmini serikali zinazokopa, taasisi za fedha na kampuni binafsi, na itaendeshwa kwa uhuru huku ikifadhiliwa kupitia mtaji wa wanahisa pamoja na mapato ya shughuli zake. Hata hivyo, AU haikutoa maelezo kuhusu wanahisa hao.
AU inasema shirika hilo linatarajiwa kusaidia nchi za Afrika kufikia masoko ya mitaji kwa urahisi zaidi, na kuwapa wawekezaji tathmini zenye uwiano zaidi na zinazozingatia mazingira halisi ya uchumi wa nchi mbalimbali barani humo.
Juhudi za kuboresha masharti ya mikopo kwa bara la Afrika zimezidi kuwa za dharura baada ya miaka kadhaa ya serikali kukopa zaidi, hali iliyozitumbukiza baadhi ya nchi katika dhiki ya madeni katika miaka ya hivi karibuni.
“Kilicho hatarini ni kikubwa,” AU ilisema, ikiongeza kuwa malipo ya kila mwaka ya madeni ya nje ya bara hilo yalipanda hadi dola bilioni 163 za Marekani mwaka 2024, kutoka dola bilioni 61 mwaka 2010. Katika nchi nyingi, malipo ya riba yamezidi bajeti za mwaka za sekta muhimu za kijamii kama afya na elimu.
“AfCRA inalenga kupunguza mizigo hiyo kwa kuongeza imani ya wawekezaji na uwazi wa masoko,” ilisema AU, ikiongeza kuwa shirika hilo pia litatathmini taasisi zisizo za Kiafrika pale inapofaa.
AU ilisema shirika hilo jipya pia linatarajiwa kupanua wigo wa tathmini, kwa kuwa nchi 23 barani Afrika hazina kiwango chochote kutoka kwa mashirika hayo matatu makubwa.
Comments
0