Mkataba uliofikiwa wiki hii kati ya serikali ya Niger na kampuni inayoendeleza miradi ya urani, Atomic Eagle, unatarajiwa kufungua milango ya ufadhili kwa miradi ya urani katika taifa hilo la Afrika Magharibi, mkurugenzi mtendaji wa kampuni hiyo aliliambia shirika la habari la Reuters.
Wizara ya madini ya Niger ilitangaza Jumatano kuwa nchi hiyo imeongeza mara mbili hisa zake katika mradi wa urani wa Madaouela hadi asilimia 40, hatua iliyohitimisha mzozo wake na kampuni ya Australia, Atomic Eagle.
Chini ya makubaliano hayo, Niger itamiliki hisa ya asilimia 15 bila kulipa gharama yoyote, pamoja na hisa nyingine ya asilimia 25 ambayo italazimika kusaidia kuigharamia ili kuendelea kuimiliki. Kwa mujibu wa mkurugenzi mtendaji, Atomic Eagle imekubali kulipia hadi dola milioni 40 za Marekani za michango ya baadaye ya Niger katika mradi huo.
Niger ni miongoni mwa wazalishaji wakubwa wa urani barani Afrika. Kwa mujibu wa takwimu za World Nuclear Association zilizotolewa Agosti, nchi hiyo ilikuwa na takriban tani 336,000 za rasilimali za urani zilizotambuliwa mwaka 2023.
Mkataba wa Madaouela ulikuja siku chache tu baada ya Shirika la Marekani la Fedha za Maendeleo ya Kimataifa (DFC) kuunga mkono mradi wa urani wa Dasa unaomilikiwa na kampuni hasimu, Global Atomic. Hatua hiyo pia imekuja wakati bei ya papo kwa hapo ya urani ikiwa juu kwa takriban moja ya tano ikilinganishwa na mwaka mmoja uliopita, ikifikia karibu dola 89.68 za Marekani kwa ratili moja (pound) mwezi Agosti, kwa mujibu wa takwimu za sekta hiyo.
Mkurugenzi Mtendaji wa Atomic Eagle, Phil Hoskins, alisema Alhamisi kuwa msaada ambao Global Atomic imeupata hivi karibuni ni “ishara nzuri mno kwamba taasisi za fedha za kimataifa ziko tayari kufadhili tena miradi ya urani ya Niger”.
Viongozi wa kijeshi walioingia madarakani kwa mapinduzi mwaka 2023 wameimarisha udhibiti wa serikali juu ya sekta ya urani ya Niger. Walifuta vibali vilivyokuwa vikishikiliwa na Orano na GoviEx (ambayo sasa ni Atomic Eagle), hatua iliyosababisha kesi za usuluhishi na kuzua wasiwasi miongoni mwa wawekezaji kuhusu utaifishaji wa rasilimali.
Hoskins alisema Atomic Eagle sasa inapanga kusasisha tafiti za upembuzi yakinifu, kupata vibali vya mazingira na kuandaa ufadhili katika kipindi cha miaka miwili ijayo, kwa lengo la kuurejesha mradi wa Madaouela katika hali ya kuwa tayari kwa ujenzi.
“Siamini kwamba (mkataba huo) una athari zozote hasi kwa uwezo wa kuendeleza mgodi au kwa uchumi wake,” alisema Hoskins, akiongeza kuwa kampuni hiyo itazingatia ufadhili kutoka kwa wawekezaji mbalimbali, ikiwemo China, inapoendelea kuusukuma mradi huo mbele.
Comments
0