Benki ya Afrika ya Uagizaji na Uuzaji Bidhaa Nje (Afreximbank) inatarajiwa kusaini siku ya Jumatatu makubaliano ya ufadhili wa dola bilioni 1.45 za Marekani kwa ajili ya kiwanda cha kwanza kikubwa cha mbolea nchini Angola. Hayo yameelezwa na kampuni inayoendeleza mradi huo, Amufert S.A., katika taarifa kwa vyombo vya habari iliyotolewa kabla ya hafla ya kusaini.
Ufadhili huo, pamoja na dola bilioni 1.19 za mtaji ambazo wanahisa tayari wameziahidi, utafikisha jumla ya uwekezaji katika mradi huo takriban dola bilioni 2.6. Huo ndio uwekezaji mkubwa zaidi kuwahi kufanyika nchini Angola nje ya sekta ya mafuta.
Kiwanda hicho cha amonia na urea kinalenga kupunguza utegemezi wa Angola kwa mbolea inayoagizwa kutoka nje ya nchi.
Mradi huo unaendelezwa na Amufert, kampuni ambayo sehemu kubwa ya hisa zake inamilikiwa na OPAIA Group, kwa ushirikiano na kampuni ya serikali Sonagas.
Ujenzi wa kiwanda unatarajiwa kukamilika mwaka 2027, na kitakuwa na uwezo wa kuzalisha tani 4,000 za mbolea kwa siku.
Kiwanda hicho kitajengwa kwenye eneo la hekta 152 mjini Soyo, karibu na pwani ya Bahari ya Atlantiki, mahali penye upatikanaji wa gesi asilia, nishati, maji na bandari ya kibiashara.
Comments
0