Kampuni ya uwekezaji wa sekta mbalimbali, Planet One Group, imetangaza kuwa itawekeza dola milioni 933 za Marekani ili kusukuma mbele uendelezaji wa mradi wa madini ya chuma wa Falémé nchini Senegal, mwenyekiti wa kampuni hiyo alisema Alhamisi.
Mradi huo wa muda mrefu, unaotekelezwa kwa ushirikiano na kampuni ya madini inayomilikiwa na serikali, MIFERSO, uko katika eneo lenye hifadhi kubwa ya madini ya chuma kusini-mashariki mwa nchi hiyo. Inakadiriwa kuwa eneo hilo lina hadi tani milioni 600 za madini ya chuma.
Kupitia tovuti yake, MIFERSO inaeleza kuwa lengo ni kuendeleza hifadhi hiyo na miundombinu yake hatua kwa hatua, hadi hatimaye kufikia kuwa na kituo kamili cha uchimbaji madini na uzalishaji wa chuma cha pua.
Planet One, yenye makao makuu yake Falme za Kiarabu (UAE), inamiliki asilimia 80 ya hisa za mradi kupitia kampuni maalum iliyoundwa kwa ajili ya mradi huo (special purpose vehicle). Mwenyekiti wake, Sanjeev Mansotra, aliiambia Reuters kuwa fedha hizo zitatolewa kwa awamu, na uwekezaji utafadhiliwa kwa uwiano wa 40 kwa 60 kati ya mtaji wa hisa na mikopo.
Serikali ya Senegal na MIFERSO kila moja inamiliki asilimia 10 ya hisa katika mradi huo.
Kwa mujibu wa Mansotra, awamu ya kwanza itagharimu takriban dola milioni 200 za Marekani, na itahusisha miundombinu na vifaa vya uchimbaji madini, pamoja na kuboresha barabara na reli.
Awamu hiyo ya awali inatarajiwa kukamilika ndani ya miezi 12 hadi 18, huku awamu ya pili ikichukua kati ya miezi 18 na 36.
“Katika awamu ya kwanza tunaangalia kuanza na tani milioni 3 hadi milioni 5 za madini ya chuma (kwa mwaka),” Mansotra alisema, akiongeza kuwa uwezo wa juu wa uzalishaji kwa mwaka unakadiriwa kufikia tani milioni 10.
Mansotra alieleza kuwa China, India na Afrika ni masoko yanayoweza kununua madini ya chuma yatakayozalishwa na mradi huo.
Katika taarifa yake, Rais wa Senegal, Bassirou Diomaye Faye, alisema mradi huo “unaakisi dhamira yetu ya kuongeza thamani zaidi kutokana na rasilimali za madini za nchi na kujenga viwanda vinavyohitajika kusaidia ukuaji wa uchumi wa muda mrefu.”
Mbali na Senegal, Planet One ina miradi mingine ya madini barani Afrika, ikiwemo lithiamu katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, boksiti nchini Guinea na dhahabu nchini Ghana.
Comments
0